Siku moja baada ya gazeti hili kuripoti habari za watoto wanadaiwa kutekwa na kufichwa katika handaki lililopo kwenye msitu wa Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, ambalo ndani yake kuna jengo kubwa lenye vyumba, Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi mkali, ana ripoti Masau Bwire.
Chanzo chetu cha habari kimedokeza kuwa, uchunguzi huo unafanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Pwani.
"Polisi wapo katika uchunguzi mkali tangu leo (jana), asubuhi, si vyema kuzitoa taarifa mapema kabla uchunguzi haujakamilika, tunaweza kuharibu upelelezi na wahusika kukimbia.
"Watoto waliokuwa wamepelekwa hospitali kuchunguzwa afya zao baada ya kuhojiwa na kutoa picha kamili ya eneo lenye handaki, hivyo uchunguzi ukikamilika mtaambiwa," kilisema chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Utekaji watoto wanaodaiwa kuwa zaidi ya 60 katika handaki hilo, unadaiwa kufanywa na raia wa kigeni (Wazungu), wakishirikiana na Watanzania ambapo watoto hao hufungiwa katika vyumba hivyo, kuteswa, kulawitiwa na kubakwa.
Watoto waliodai kutoroka kwenye handaki hilo ni Emmanuel Robert (11) anayesoma darasa la tano Shule ya Msingi Maendeleo iliyopo Tabata, Segerea, Dar es Salaam na mdogo wake Godianus Robert (8), anayesoma darasa la tatu shuleni hapo.
Watoto hao walidai kutekwa na Wazungu wawili asubuhi ya Septemba 2 mwaka huu, wakati wakienda shuleni na kufanikiwa kutoroka katika jengo hilo Septemba 23 mwaka huu.
Wakiwa wamechoka na afya zao kuzorota katika Kituo kidogo cha Polisi, Kibaha Maili Moja, mkoani Pwani, watoto hao walisema ndani ya jengo hilo kuna watoto wengi wa kike na kiume.
Walisema watoto hao wanafanyishwa kazi na kuteswa kwa kutandikwa fimbo, kuchomwa moto na kupigwa shoti ya umeme hasa wanapowaulizia wazazi wao ambapo baadhi yao hubakwa na kulawitiwa.
Akizungumza na Majira, Emmanuel alisema baada ya kutekwa yeye na mdogo wake, walifungwa na vitambaa vyeusi usoni hadi walipofikishwa ndani ya jumba hilo la mateso.
Aliiomba Serikali kufanya jitihada za hali na mali ili kuwaokoa watoto wengine waliopo katika jengo hilo.
Mama mzazi wa watoto hao, Martha Godianus (29), ambaye anafanya shughuli za mama lishe, njia panda ya Barakuda, Tabata Manispaa ya Ilala, alisema amehangaika zaidi ya miezi mitatu kuwatafuta watoto hao bila mafanikio.
Juzi Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei alikiri kupata taarifa za tukio hilo na kuanza kuzifanyia kazi.
Source: Majira