16 January 2014

Dar es Salaam
Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam, wanatajwa kuwa wahusika wakuu wa kusaidia wahamiaji haramu kuingia nchini, kinyume cha sheria.
Septemba mwaka jana, mfanyakazi wa Wakala wa Ndege za Serikali, Dominic Bomani alimwambia Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alipotembelea uwanjani hapo kuwa wapo wahamiaji haramu ambao wamepewa nafasi nyeti za ajira katika uwanja huo. Dk Mwakyembe aliahidi kufuatilia suala hilo.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa polisi katika baadhi ya viwanja vya ndege wamejenga mtandao na watumishi wengine, wakiwamo wa Idara ya Uhamiaji ambao huwawezesha raia wa kigeni hasa kutoka nchi za Ethiopia, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), kuingia nchini bila ya kuwa na nyaraka zinazokubalika kisheria.
Tukio la karibuni zaidi ni lile la kuingizwa nchini kwa raia watatu wa Pakistani ambao licha ya kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa zamani (Terminal – I) kutokana na kutokuwa na hati za kusafiria, wala nyaraka zozote zinazowaruhusu kuingia nchini, baadaye waliachiwa na kuingia nchini katika mazingira ya kutatanisha.
Chanzo chetu uwanjani hapo kilisema: “Hawakuja na hati za kusafiria wala nyaraka zozote na waliachiwa huru katika mazingira ya kutatanisha.”
Chanzo hicho kiliwataja Wapakistani hao kuwa ni Hussein Amir, Ahmad Tahmir na Shakeel Muhamadadi ambao walifika nchini, Oktoba Mosi, 2013 saa kumi na moja jioni kwa ndege ndogo ya kukodi ambayo ilikuwa ikitokea Zanzibar.
Baada ya kufika, walishukia Terminal 1 na baadaye kwenda kuswali katika msikiti wa karibu, lakini kabla ya kutimiza azma yao hiyo, walikamatwa na polisi kisha kufunguliwa hati ya kukamatwa (RB) namba JNIA/1005/2013.


Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment