Baadhi ya nyaraka alizokamatwa nazo ofisa usalama feki.
Kushoto ni Ofisa Usalama feki, Bw. Alquine Masubo,akiwa polisi.
SIKU chache baada ya trafiki feki mwenye cheo cha sajini kukamatwa jijini Dar es Salaam akiongoza magari, mapya yamezidi kuibuka baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kufanikiwa kuwakamata watu saba wanaotuhumiwa kuwa majambazi wakiwa wamevalia sare za jeshi hilo wakiwa na vyeo tofauti.
Mbali watu hao, Polisi pia amemkamata mkazi mwingine wa jijini Dar es Salaam akijifanya Ofisa wa Usalama wa Taifa, huku akiwa na nyaraka mbalimbali za Serikali kutoka Ofisi za Uhamiaji na kitambulisho chake cha kazi, ambacho alikuwa akikitumia kabla ya kustaafu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Pia alikamatwa na bastola mbili zikiwa na risasi 12 na baada ya kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake alibainika kumiliki bastola nyingine ya tatu ikiwa na risasi 19.
Kukamatwa kwa watu hao kulithibitishwa na Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana.
Alisema katika tukio la kwanza Polisi walifanikiwa kukamata watu saba wanaodaiwa kuwa majambazi wakiwa wamevalia sare hizo, huku mmoja akiwa na cheo cha Meja ambapo sare yake ilionesha beji inayosomeka SSGT A.M Mduvike.
Source: Majira
No comments:
Post a Comment