Dar es Salaam.
Siri imefichuka ya jinsi gani mtu ambaye aliyejifanya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, James Juma Hussein (45), alivyokamatwa wakati akiwa ‘kazini’ eneo la Kinyerezi Mnara, Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi na kuthibitishwa na mmoja kati ya askari walioshiriki katika kumkamata zinabainisha kuwa mtuhumiwa huyo ambaye anatarajiwa kupandishwa kizimbani leo (Jumatatu), alitiwa mbaroni baada ya kulisimamisha gari binafsi la mmoja kati ya makamishna wa polisi.
Inadaiwa kuwa siku ya tukio askari huyo alisimamisha gari la bosi huyo wa polisi ambaye alitii sheria na kabla ya maelezo zaidi kutoka kwa askari huyo feki wa usalama barabarani, mkuu huyo alijitambulisha kwa askari huyo.
Askari huyo wa Kituo cha Stakishari alisema: “Inapotokea askari mwenye cheo cha juu anapojitambulisha pengine kwa kuwa hukumfahamu kabla, kinachofuata ni saluti kabla ya kumruhusu kuendelea na safari lakini kitu hicho hakikufanyika hali ambayo ilimfanya bosi huyo akasirike.
Kinaeleza chanzo hicho kuwa askari waliotumwa kumfuatilia walipofika eneo hilo kwa ajili ya kumtambua na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kosa alilofanya, waliposimamisha gari na kumuita alitimua mbio kabla ya kutiwa mbaroni na kujifanya amepoteza fahamu mara baada ya kumdaka.
Askari hao walimbeba na kumpandisha katika gari ‘defender’ hadi Kituo cha Polisi Stakishari ambako amefunguliwa jalada la kujifanya askari wa usalama barabarani akijua kuwa si kweli na atafikishwa mahakamani leo kujibu mashtaka yanayomkabili.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment