31 July 2012

CHADEMA: ZITTO ACHUNGUZWE

LISSU ATAJA WABUNGE WALA RUSHWA

Na Edson Kamukara, Dodoma



KAMBI rasmi ya Upinzani Bungeni imetaka kuchunguzwa kwa madai ya Naibu Kiongozi wa wa kambi hiyo, Zitto Kabwe, kuhongwa.

Kambi hiyo pia imetaja majina ya wabunge sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, mwishoni mwa wiki, ikidai kuwa kwa namna moja ama nyingine walihusika na vitendo vya rushwa.

Wabunge hao wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa kampuni za mafuta ili kuipigia debe menejimenti ya Shirika la Ugavi wa umeme nchini (TANESCO).

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Mnadhimu Mkuu wa kambi hiyo, Tundu Lissu, alisema wamesikia tuhuma nyingi dhidi ya Zitto lakini hawajamhoji kiongozi huyo.

Alisema wanaviomba vyombo vinavyohusika vimchunguze Zitto ili ukweli ujulikane na hatua zinazostahili zichukuliwe kama atathibitika kuwa na makosa.

“Chama hatujakaa na Zitto kumsikiliza lakini tunataka achunguzwe, hatuna masilahi yoyote katika uchafu huu wa rushwa. 

“Uchunguzi huu utatupa msingi wa kumchukulia hatua kama chama ikiwa itathibitika amehongwa,” alisema.


Alibainisha kuwa, mbunge wao huyo amekuwa akihusishwa na kumtumia ujumbe mfupi wa vitisho Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakimu Maswi.

Alisema ni vema Zitto achunguzwe na apewe nafasi ya kujieleza kama itakavyokuwa kwa wengine kuliko kuendelea kusambaza maneno ya kufikirika.

Alibainisha wamejiridhisha pasipo shaka kuwa wabunge wao watatu waliokuwa wajumbe kwenye Kamati ya Nishati na Madini, John Mnyika (Ubungo), David Silinde (Mbozi Magharibi) na Mwanamrisho Taratibu Abama (Viti Maalumu), hawajahusika kwa lolote katika sakata hilo la rushwa.

“Kama kuna mtu ana ushahidi zaidi ya huu tulionao tunaomba atuletee ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa, lakini mpaka sasa wabunge wetu hawa watatu hawajashiriki kwa lolote katika kuomba rushwa,” alisema.

Kauli ya Lissu inashabihiana na aliyoitoa Zitto juzi ambapo alisema hajachukua hongo, ila kuna watu wana lengo la kuchafua jina lake.

Zitto alisema kuwa uchunguzi dhidi yake ndiyo njia pekee ya kuudhihirishia umma kuwa hahusiki na chochote kama baadhi ya watu wanaoeneza maneno ya kumchafua.

Awataja wala rushwa

Kuhusu majina ya wabunge wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, Lissu alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, wabunge hao walipaswa kutaja masilahi yao kibiashara kwenye shirika hilo.

“Sasa wabunge hawa hawajawahi kufanya hivyo na wameendelea kuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini na wengine kufanya biashara na TANESCO,” alisema Lissu na kuwataja kuwa ni Munde Tambwe, Sara Msafiri, Mariam Kisangi wa Viti Maalumu, Yusuf Nassir (Korogwe Mjini) na Charles Mwijage Muleba Kaskazini.


soma zaidi Tanzania Daima





source: TANZANIA DAIMA, 31st July,2012





I'm not a big fun of siasa, laikini hii habari imenichosha!!!! mmmh!

No comments:

Post a Comment