18 November 2013

KASHFA YA KUMBAKA BINTI - MBUNGE WA URAMBO MAGHARIBI, Prof. JUMA KAPUYA

Juma Kapuya

KASHFA ya kumbaka na kutishia kumuua msichana wa miaka 16 inayomkabili Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), imezidi kuchukua sura mpya baada ya serikali kutoa kauli nzito ya kutaka kumfungulia mashitaka mbunge huyo, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Mashitaka yanayotajwa kumkabili mbunge huyo ambaye amepata kuwa waziri katika awamu tofauti za uongozi, ni pamoja na ubakaji na kutishia kuua.
Kamishna  wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliliambia gazeti hili jana kuwa jeshi hilo halitakuwa na sababu ya kumuacha mbunge huyo kuendelea kutamba mitaani huku akituma ujumbe wa vitisho kwa binti wa miaka 16  anayedaiwa kumbaka.
Alisema watachukua hatua za haraka  kama mtoto huyo atakwenda kufungua jalada la kutishiwa maisha katika kituo chochote cha polisi jijini Dar es Salaam wakati wowote.
Kamishna Kova alisema hadi jana jeshi lake lilikuwa halijapata malalamiko yoyote kutoka kwa binti anayedai kubakwa na kutishiwa maisha na Profesa Kapuya, kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi iliyosajiliwa kwa jina la Profesa Kapuya na kuongeza kuwa muda wowote taarifa hizo zitakapofikishwa polisi wataanza kuzifanyia kazi.
“Sisi Polisi hatuna shamba hapa mjini zaidi ya kukabiliana na uhalifu… na huyo binti mwambie aje afungue malalamiko yake, tena amuone RPC yeyote katika mikoa ya kipolisi ya Dar es Salaam na si hili la kutishiwa tu, hata hilo analosema la kubakwa na sisi tutamuwajibisha aliyefanya hivyo katika makosa mawili tofauti,” alisema Kamishna Kova.
Wakati Kamanda Kova akisema hawatakuwa na ajizi na tuhuma za kubaka na kutishia kuua zinazomkabili Profesa Kapuya, habari kutoka Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete zinaeleza kuwa kiongozi huyo wa nchi amekerwa na kauli ya Mbunge huyo wa Urambo Magharibi kuwa serikali haiwezi kumfanya jambo lolote.
Ni kutokana na kauli hiyo mtoa taarifa wetu alisema rais aliagiza vyombo vya dola kufuatilia kwa karibu sakata hilo na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake.Juzi gazeti hili lilinukuu moja ya ujumbe mfupi wa maneno kutoka katika simu ya Profesa Kapuya kwenda kwa binti anayedai kubakwa na Kapuya, sehemu ya ujumbe huo unasomeka kuwa: “Mkiuawa itakuwa vizuri….itawapunguzia gharama za kuishi, usitake kugombana na serikali mtoto mdogo kama wewe, sisi ndiyo wenye nchi yetu, mwenye hilo gazeti ni Mbowe, sasa mwambieni nyumba ya kuishi si mmemuingizia hela leo? Mnatumika tu bure watu wanaingiza hela nyingi, ila mmenitibua lazima niwaue wiki hii haitaisha nitapiga kambi kote, jana si wamekuficha, tuone utalindwa milele, maana washatengeneza hela lazima mvae sanda tu, hilo sio ombi ni wajibu wenu, mnajitia na nyie mafia watoto siyo, watoto wetu wanauza unga nani anawakamata? Nani atapingana  nasi.”
Pia kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), taarifa zinaeleza kuwa chama hicho kimeamua kumtosa mbunge huyo aliyewahi kuongoza Wizara ya Elimu na Ulinzi kwa nyakati tofauti baada ya kumtaka aache kukihusisha chama na kashfa yake ya kubaka.
Mmoja wa viongozi wa CCM  aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotaja jina lake kwa vile siye msemaji wa chama, alidokeza kuwa chama hicho kilijaribu kulimaliza suala hilo kimya kimya, lakini lilikwamishwa na Profesa Kapuya mwenyewe kwa kutofika kwenye vikao vya usuluhishi na binti huyo.
Pia imebainika kuwa baadhi ya wabunge waliokuwa wanataka kumsitiri Profesa Kapuya aliishia kuwaona kama wabaya wake.
“Hapa palipofika ahangaike peke yake, watu walijitahidi kadiri walivyoweza hili suala limalizike lakini mwenzetu alikuwa mzito kushirikiana nasi, sasa hakuna anayetaka chama kichafuke zaidi, amesubiriwa Dodoma na watoto wiki mbili  hatokei, hadi watoto wakashauriwa kwenda kuwaona viongozi wakuu Dar es Salaam,” alisema kiongozi huyo.
Juzi gazeti hili lilichapisha habari kuhusu mwanafunzi huyo aliyesema kuwa waziri huyo alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo ndani ya ofisi yake katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipoitwa kwenda kuchukua ada kwa mara ya pili.
Kutokana na habari hiyo Profesa Kapuya kupitia kwa wakili wake, Yasin Memba, alitishia kuliburuza gazeti hili mahakamani endapo halitamwomba msamaha ndani ya siku saba.
Mbali na kutishia kulipeleka gazeti hili na baadhi ya mitandao ya kijamii mahakamani pia Profesa Kapuya alikana kumfahamu binti anayedai alibakwa huku akikanusha  kumiliki simu namba 0784993930 ambayo imekuwa ikitumiwa kuwasiliana naye ikiwemo kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms) wa vitisho.


Source: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment