16 January 2014

Mijimama’ inavyoingiza waosha kucha, miguu katika hatari ya kuambukizwa VVU



Utengenezaji wa kucha na uoshaji miguu ni biashara inayokuwa kwa kasi hasa maeneo ya mijini ambapo wanawake wengi wanahusudu na kujihusisha na masuala ya urembo.
Biashara hii inazidi kukua huku pia huduma zinazotolewa zikizidi kuongezeka kila kukicha, ambapo mara nyingi wanaotengeneza kucha, hujihusisha na usuguaji wa miguu, uchoraji wa tattoo ukandaji wa mwili (massage) na nyingine zinazofana na hizo.
Kazi hii imetokea kuwa chanzo kimojawapo cha mapato na ajira mpya kwa vijana wengi hasa wa kiume, wenye umri wa miaka 17 hadi 35.
Hata hivyo, uchuguzi uliofanywa na gazeti hili hasa jijini Dar es Salaam, umegundua kuwa vijana wengi wanaofanya biashara hii huishia kufanya ngono na wateja wao hasa wanawake wenye umri mkubwa na wa kati (Mijimama), ambao wamewahi kuwahudumia zaidi ya mara moja, hivyo kutumbukia katika hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa na Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Kwa mujibu wa takwimu za Ukimwi nchini, vijana wengi walio kwenye umri  kati ya miaka 17 hadi 35 ndilo kundi linalotajwa kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU.
Hatari hiyo inatokana na mazingira hatarishi wanayokutana nayo vijana hao wanapofanya shughuli zao na kufanya vitendo hivyo kwa makusudi, wakati mwingine kwa kushawishiwa.
Uchunguzi unaonyesha kuwa wakati wa ufanyaji wa shughuli hiyo, hutokea baadhi ya wanawake wakaoshwa au kusuguliwa sehemu za miguu zinazokaribia maeneo ya mapaja, hivyo kuamsha hisia kati ya mtoa huduma na mpokea huduma.
Hatua hiyo inatajwa kuwasababashia baadhi yao kufanya ngono ambayo mara nyingi siyo salama, wanapotoa huduma katika maeneo tulivu ikiwamo saluni maalumu na  nyumbani kwa wateja.
Mmoja wa wafanyabiashara hiyo katika Soko la Mwenge Hamis Shaban(19) (siyo jina halisi) anasema kuwa kuna wakati wamekuwa wakiingizwa katika mtego na wateja wao, ambayo huwasababishia kufanya ngono.
Anasema kuwa hali hiyo hutokea mara nyingi hasa mteja anapotaka kwenda kuhudumiwa nyumbani kwake, ambapo hukuta tayari wameandaa mazingira, ambayo mwisho wake huishia katika hatua hiyo.
“Mimi mwenyewe imenitokea siku chache zilizopita; kuna binti fulani amekuwa mteja wangu kwa muda mrefu, amekuwa akinifanyia vituko vya hapa na pale. Nilikuwa sijali, ila majuzi akaniambia niende kwake nikamchore tattoo,” anasema Shaban na kuongeza:
“Eneo alilotaka nimchore ndilo lilianza kunipa wasiwasi, lakini kwa sababu ya pesa nikapiga moyo konde. Akavua blauzi yake na kutaka nimchore kwenye titi; nilijaribu kutimiza wajibu wangu, lakini mambo ambayo alikuwa akifanya, yalinisababishia uzalendo kunishinda, hatimaye tukajikuta tukifanya ngono.”

Na Elizabeth Edward

Source; Mwananchi

2 comments:

  1. Daahh...sasa itakuwaje kwa wale tunao-osha kucha??!! maana hata wanaume siku hizi wanaoshwa kucha..ngoma inogile..(shosti)

    ReplyDelete
  2. hahaaaha! ndio maana yake shosti, ni kuwa makini tu! tena haswa massages!

    ReplyDelete