24 May 2013


Laana ya gesi

•  POLISI WAMPIGA RISASI MJAMZITO, WAIBA VITU


 UGUNDUZI wa gesi asilia mkoani Mtwara umegeuka laana kwa wakazi wake wanaoishi maisha ya wasiwasi hivi sasa.

Sauti za milio ya mabomu, risasi, na vipigo ndivyo vinavyonekana kushamiri zaidi kwenye mji huo uliosifika kwa amani na utulivu kwa muda mrefu.

Tanzania Daima lilishuhudia idadi kubwa ya askari polisi na wanajeshi wakiwa kwenye pikipiki na magari wakizunguka maeneo mbalimbali kwa lengo la kudhibiti vurugu.

Wakati hali ikizidi kuwa tete mkoani humo, jana polisi wanadaiwa kumuua kwa kumpiga risasi mjamzito aliyekuwa nyumbani kwake eneo la Magomeni.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi amethibitisha kupokea mwili wa mjamzito huyo ukiwa na tundu tumboni, na hivyo kufanya idadi ya maiti zilizopokelewa hospitalini hapo kufikia mbili na majeruhi 18.

“Ni kweli kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi saba, amepigwa risasi tumboni.
“Pia tumepokea mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Chuno, amevunjwa miguu yote kwa risasi,” alisema Dk. Ligula.

Habari ambazo Tanzania Daima ilizipata kutoka Mtwara jana, zilidai polisi walishiriki kuchoma moto nyumba tatu za wananchi katika eneo hilo na vibanda vya maduka kadhaa na kupora vitu vilivyomo ndani.

Chanzo kimoja kimedokeza kuwa maeneo ya Magomeni, Chikongola, Nkanaledi na Mikindani, askari walikuwa wakiingia kwenye nyumba za watu na kumkamata mtu yeyote hususan wanaume.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa uhalifu uliofanywa na askari hao uliamsha hasira za wananchi jambo lililosababisha kutokea mapambano kati yao.

Baadhi ya vitu vinavyodaiwa kuibwa na askari hao kutoka kwenye maduka ni mchele, sukari, unga wa ngano na nguo.
Wakati polisi wakidaiwa kushiriki kwenye vitendo hivyo, huduma za kijamii zimesimama hali inayochangia mambo kuzidi kuwa tete ndani ya mkoa huo.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wakazi wa Mtwara wamelalamikia kitendo cha askari wa Jeshi la Polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga na kuwapora mali zao.

“Magomeni A hatuna amani, askari wanaingia majumbani mwetu, wanatupiga na kutunyang’anya simu, yaani huku Magomeni hatuna amani kabisa, tumepoteza watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi,” alisema Paulina Idd.

“Majumba yetu yamechomwa moto wanaofanya fujo ni polisi wenyewe halafu wanakuja wanatubaka na kuiba mali zetu, tunateseka sisi, yaani tumechoka kabisa na serikali yenyewe,” aliongeza kusema.

Wakati wananchi wakilalamikia hali kutokuwa shwari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema hali ni nzuri na kuwataka wakazi wake waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Alipoulizwa kuhusu polisi kumuua mjamzito, kuchoma moto nyumba na kuiba vitu, kamanda huyo alikataa kuyazungumzia hayo kwa madai atapingana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Kamanda Sinzumwa alisema jana walimtarajia Waziri Nchimbi mkoani humo ili kuangalia hali ya mambo.


Wakazi wakimbia maeneo yao

Wakazi wa maeneo mbalimbali mjini Mtwara wamekimbia makazi yao hususani wanawake na watoto na kuhamia hospitali ya rufaa kwa kuhofia usalama wao huku wengi wao wakipotezana na ndugu zao.

Hali hiyo imetokea kufuatia kuwepo kwa milipuko ya mabomu katika maeneo mbalimbali mjini humo huku huduma za kijamii zikiwa bado zimesitishwa.



SOURCE: Mtanzania



No comments:

Post a Comment