26 June 2012

AKAMATWA NA KICHWA CHA ALBINO


MFANYABIASHARA wa baa na nyumba ya kulala wageni ya Bongo Star Lodge iliyopo Kawe Ukwamani, James Isame, maarufu kama Mzee Chacha (50), anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni kwa tuhuma ya kukutwa na kichwa cha binadamu anayedhaniwa kuwa ni mlemavu wa ngozi (albino).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela amethibitisha kushikiliwa kwa mfanyabiashara huyo na kusema kuwa alikamatwa juzi saa 2:45 usiku baada ya wasamaria wema kutoa taarifa kwa jeshi hilo juu ya kuwepo kwa tukio lisilo la kawaida katika nyumba hiyo ya kulala wageni.

Alieleza kuwa, baada ya taarifa hizo, polisi waliizingira nyumba hiyo kisha wakamtafuta mjumbe wa eneo la Kawe kwa ajili ya kuthibitisha upekuzi utakaofanyika na kwamba baada ya taratibu zote, walimtaarifu muhusika ambaye alianza kuonesha upinzani juu ya kufanyiwa upekuzi.

Alisema jitihada za mtuhumiwa kuzuia upekuzi huo zilishindikana, ndipo katika kufanya kazi hiyo maeneo yote ya ndani na nje ya nyumba hiyo pamoja na baa, walifanikiwa kukuta kichwa cha binadamu kikiwa kimewekwa juu ya ukuta wa choo.

“Kilikuwa kimevingirishwa katika mfuko wa rambo na tuliweza kubaini kuwa ni kichwa cha binadamu baada ya kuona nywele na meno, ila bado hatujajua ni wa jinsia gani au kama ni mlemavu wa ngozi,” alisema Kenyela.


Na Abdallah Khamis
SOURCE: TANZANIA DAIMA, 25/6/2012


HIVI KUMBE BADO KUNA WENYE UPUNGUFU WA AKILI  WANAO AMINI KUHUSU KUUA BINADAMU WENZAO KWA AJILI YA MALI? TUTAENDELEA KWELI KWA MWENDO HUU ?

No comments:

Post a Comment